NI DHAMIRA YA SERIKALI KULIPA FIDIA WANANCHI WANAOPISHA MIRADI YA MAENDELEO- MHE. KAPINGA

 


📌 *Ataja fidia iliyolipwa kwa baadhi ya miradi ya umeme*


📌 *Aeleza mipango ya ujenzi wa vituo vya kujazia gesi kwenye magari (CNG)*


Naibu Waziri Nishati, Mhe Judith Kapinga amesema ni dhamira ya Serikali kuhakikisha kuwa wananchi wote wanaopisha miradi ya maendeleo wanalipwa fidia kulingana na taratibu zilizopo.


Mhe. Kapinga ameyasema hayo leo Oktoba 30, 2024 bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mhe. Silvestry Koka, Mbunge wa Kibaha Mjini aliyetaka kufahamu ni lini Serikali italipa fidia kwa Wananchi na kampuni zipatazo 18 zilizopo kwenye eneo la viwanda la Zegereni Mji wa Kibaha mkoani Pwani ambao wamepitiwa na njia ya umeme ya kV 400.


Mhe. Kapinga ameeleza kuwa, Serikali imelipa fidia awamu ya kwanza kwa takriban shilingi bilioni 29.4 kati ya shilingi Bilioni 33 zinazotakiwa kulipwa kwa wananchi wanaopisha mradi huo wa njia ya kusafirisha umeme msongo wa Kilovoti 400 kutoka Chalinze hadi Mkuranga mkoani Pwani.


"Katika eneo la viwanda la Zegereni kuna wananchi na kampuni 18 ambao wanadai fidia yenye thamani ya Shillingi billioni 1.1. Serikali inaendelea kulipa fidia hizi kadri fedha inavyopatikana." Amesema Mhe. Kapinga


Akijibu swali la Mbunge wa Lupembe, Mhe. Edwin Swalle aliyeuliza ni lini Serikali itawalipa fidia wananchi wa Kata ya Kichiwa eneo la Idumila na eneo la Luhuji Idamba, Mhe. Kapinga amesema wananchi hao watafanyiwa tathmini ili kuweza kulipwa fidia.


Aidha, akijibu swali la Mbunge wa Makete, Mhe. Deo Sanga aliyetaka kufahamu ni lini Serikali itawalipa fidia wananchi wa Makete waliopisha ujenzi wa mradi wa kuzalisha umeme wa Rumakali, Mhe. Kapinga amesema fidia kwa Wananchi wanaopisha mradi huo ni takriban shilingi bilioni 27 na taratibu za kulipa fidia hiyo zinaendelea.


Aliongeza kuwa, kukamilika kwa miradi ya Rumakali na Ruhudji kutakwenda kuzalisha takriban megawati 580 za umeme.


Akijibu swali la Mbunge wa Donge, Mhe. Soud Mohamed Juma aliyetaka kujua mkakati wa Serikali kuimarisha upatikanaji wa huduma ya gesi kwa matumizi ya magari na mitambo nchini, Mhe. Kapinga amesema Serikali ilishaanza programu mbalimbali za matumizi ya gesi iliyogandamizwa (CNG) kwenye magari.


Ameongeza kuwa, Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi imefanikiwa kufungua vituo 5 vya CNG na inatarajia kufungua vituo vingine 3 ifikapo mwezi Desemba, 2024.


Aidha, jumla ya vituo 13 (vituo mama 2, vya kuhamishika 6 na vituo vidogo 5) vinatarajiwa kufunguliwa mwaka 2025.


Kuhusu kupanua wigo wa upatikanaji wa CNG, alisema Serikali imeshaanza kufanyia kazi suala hilo kwa baadhi ya vituo vya kuhamishika kuwekwa mkoani Dodoma na tathmini imeshaanza kufanyika.


Amesema mikakati inaendelea ili kuhakikisha pande zote za Muungano zinanufaika na rasilimali iliyopo.

Post a Comment

0 Comments