MWANAMKE ACHOMWA NA KUTOBOLEWA MACHO NA MTALAKA WAKE, POLISI SHINYANGA KUMSAKA MTUHUMIWA




Kamanda wa jeshi la polisi Mkoa wa Shinyanga kamishna msaidizi mwandamizi wa Polisi (SACP) Janeth Magomi akitoa taarifa ya tukio hilo.


Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga linamsaka mwanaume anayefahamika kwa jina la Paul, mkazi wa mtaa wa Banduka, kata ya Ndala, Manispaa ya Shinyanga, kwa tuhuma za kumjeruhi vibaya mtalaka wake, Bi. Ester Matalanga, kwa kumtoboa Macho.


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Kamishna Msaidizi Mwandamizi Janeth Magomi, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo akieleza kuwa, "Siku ya tarehe 13, Mwezi wa 8, 2024, majira ya saa kumi na moja na nusu alfajiri, nilipokea simu kutoka kwa Mwenyekiti wa mtaa wa Banduka akiniarifu kwamba kuna mwanamke ametobolewa macho na mtu anayesadikika kuwa ni mume wake wa zamani.".


"Kwa haraka kabisa, jeshi la polisi lilimchukua mwanamke huyo na kumpeleka Hospitali ya Kolandoto kwa ajili ya matibabu ambapo uchunguzi wa awali unaonyesha kwamba tukio hili chanzo chake ni wivu wa mapenzi, na mtuhumiwa ni mlinzi anayefanya kazi Buhangija., hatuwezi kuvumilia ukatili huu, na tutahakikisha mtuhumiwa anafikishwa kwenye vyombo vya sheria."amesema Kamanda Magomi


Mwenyekiti wa mtaa wa Banduka, Bw. Pius Mathias, ameeleza kwamba alipata taarifa kutoka kwa wakazi wa mtaa wake usiku wa kuamkia jana ambapo alifanya juhudi za kuwasiliana na polisi.


“Usiku wa kuamkia jana majira ya saa tisa usiku nilipigiwa simu na wananchi wangu wanaoishi karibu na bondeni pale mtoni kwamba kuna mwanamke ametobolewa macho sikuchelewa nikawa nimefika kwenye eneo la tukio ni kweli nikamkuta huyo mwanamke ambaye alikuwa akijieleza lakini kwa simanzi alikuwa haoni tayari alikuwa ametobolewa macho yake yote basi baada ya kuona tukio hilo ikabidi nipige simu polisi”


"Nashukuru Kamanda wa Polisi Mkoa alitoa ushirikiano wa kutosha, na maafisa wake walifika haraka eneo la tukio na kumsaidia mwanamke huyo," amesema Mwenyekiti Pius


Wakazi wa mtaa wa Banduka wameeleza masikitiko yao juu ya ukatili huo na kuzitaka mamlaka husika kuchukua hatua kali dhidi ya mtuhumiwa ili kuhakikisha haki inatendeka.



Mwenyekiti wa mtaa wa Banduka, Bw. Pius Mathias, akizungumzia tukio hilo.

Picha ya Bi. Ester Matalanga

Post a Comment

0 Comments