Afisa Mtendaji wa Kata ya Segese Apongeza Juhudi za FaDev Katika Kupambana na Madhara ya Zebaki




Na Paul Kayanda, Kahama.


Afisa Mtendaji wa Kata ya Segese, Halmashauri ya Msalala wilayani Kahama, mkoani Shinyanga, Patrick John Mahona, amepongeza juhudi zinazofanywa na Taasisi ya Kuendeleza Uchimbaji Mdogo Tanzania (FaDev), chini ya Mkurugenzi wake, Mhandisi Christina Mwasa, katika kusambaza elimu kuhusu madhara ya zebaki kwenye vijiji, mashuleni, na Halmashauri nzima ya Msalala.


Eneo hilo linatajwa kuwa na hatari kubwa ya athari za zebaki kutokana na kuzungukwa na migodi mbalimbali, ikiwemo mialo ya kuchenjulia dhahabu.


Mahona aliyasema hayo leo wakati wa ufunguzi wa semina iliyofanyika Segese, iliyowahusisha maafisa watendaji wa kata na vijiji, pamoja na baadhi ya wachimbaji kutoka migodi midogo ya Wisolele.


Katika hotuba yake, Mahona aliomba viongozi wa FaDev kutumia fursa ya matamasha mbalimbali, hususan michezo ya mpira wa miguu inayoendelea kwenye kata ya Segese, kufikisha ujumbe wa madhara ya zebaki kwa umati mkubwa wa watu wanaohudhuria matamasha hayo.


Naye Mkurugenzi wa FaDev, Mhandisi Christina Mwasha, alielezea madhara ya zebaki na juhudi wanazozifanya kutokomeza matumizi yake. Alisisitiza umuhimu wa kuelimisha wachimbaji wadogo ili kupunguza matumizi ya zebaki ifikapo mwaka 2030, kwa angalau asilimia 30, au hata kutokomeza kabisa.


"Tunawahimiza wachimbaji kutumia zebaki kwa tahadhari, kama ilivyo kwa magonjwa ya UKIMWI na Covid-19, ili kuepuka madhara makubwa ya kiafya na mazingira," alisema Mwasha.

Post a Comment

0 Comments