Afisa Mtendaji wa Kata Apendekeza Tamasha la Mpira Kutumika Kutoa Elimu ya Kupambana na Madhara ya Zebaki




Na Paul Kayanda, Kahama


Afisa Mtendaji wa Kata ya Segese, Halmashauri ya Msalala, wilayani Kahama Mkoani Shinyanga Patrick Mahona, ameshauri kutumia tamasha la mpira wa miguu aliloliandaa kama jukwaa la kutoa elimu kwa jamii kuhusu madhara ya zebaki.


Ushauri huo ulitolewa jana kwenye semina iliyoshirikisha wachimbaji wadogo wa madini ya dhahabu,viongozi wa vijiji,vitongoji vya Wisolele kata ya Segese,wakiwemo maafisa watendaji wa vijiji hivyo na kata iliyolenga kuwapa wananchi uelewa wa kina kuhusu athari za kemikali hiyo hatari.


Mahona alieleza kuwa tamasha hilo la mpira wa miguu, linalokusanya watu wengi hasa vijana, ni fursa nzuri ya kufikisha ujumbe kwa jamii kwa njia iliyo rahisi kueleweka na ya kufurahisha. "Tamasha la mpira linavutia watu wa rika zote, na ni nafasi nzuri ya kutoa elimu kuhusu namna ya kujikinga na madhara ya zebaki, hasa katika maeneo yanayohusika na uchimbaji wa madini," alisema Mahona.


Katika semina hiyo, wananchi walihimizwa kuepuka matumizi ya zebaki katika shughuli za uchimbaji wa madini, huku wakipewa mbinu mbadala na salama za kuepuka athari zake. Tamasha hilo, linalotarajiwa kufanyika wiki ijayo, linatarajiwa kuwa na michezo mbalimbali, huku vikundi vya afya na wataalamu wakishirikiana kutoa elimu kwa njia ya burudani.


Hatua hii ya Mahona inaonesha nia yake thabiti ya kupambana na madhara ya zebaki kwa kutumia mbinu za kibunifu na zinazohusisha jamii nzima, kwa lengo la kulinda afya na ustawi wa wakazi wa Segese na maeneo jirani.

Post a Comment

0 Comments