MTOA TAARIFA NA SHAHIDI ANALINDWA-DKT.MWINYI



Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi amesema tayari Tanzania imeanza kutumia sheria ya mwaka 2015 sura ya 446 katika kumlinda Mtoa Taarifa na Mashahidi kwa makosa mbalimbali yaliyoshuhudiwa yakitendeka kwa kuwapatia ulinzi wa kisheria watoa taarifa ili kuongeza mapambano ya uhalifu nchini.


Rais Dkt.Mwinyi aliyasema hayo wakati wa Maadhimisho ya siku ya mapambano dhidi ya rushwa Afrika katika ukumbi wa kimataifa wa maonesho ya biashara Nyamanzi, Mkoa wa Mjini Magharibi tarehe 11 Julai 2024.


Aidha Rais Dkt.Mwinyi amesema sheria ya kumlinda mtoa taarifa itasaidia ulinzi, kuwapa motisha na kulipa fidia kwa watoa taarifa pamoja na mashahidi ili kuwaongezea imani na kuimarisha usalama wa maisha yao.


Vilevile Rais Dkt.Mwinyi ameeleza kuwa mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi wa mali za umma ni kipaumbele cha Serikali katika kuchochea malengo ya maendeleo yaliyokusudiwa .


Kwa upande mwingine Rais Dkt.Mwinyi amezipongeza jitihada za Taasisi ya ZAECA na TAKUKURU kwa mapambano dhidi ya rushwa na uhujumu uchumi nchini, pia ametoa wito wa kuendeleza jitihada za mapambano ya rushwa nchini.

Post a Comment

0 Comments