MARUFUKU KUTOA KADI ZA HOMA YA MANJANO KIMAGENDO BILA KUCHANJA







Na WAF - KIGOMA


Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Tumaini Nagu amekemea na kulaani vikali Tabia ya baadhi ya watoa huduma za Afya mipakani wasio waadilifu kuuza au kutoa kadi za homa za manjano kwa magendo kwa watu ambao hawajachanjwa.


Prof. Nagu amesema hayo Julai 16, 2024 wakati wa ziara yake Mkoani Kigoma ambapo ametembelea bandari ya Kibirizi na bandari ya Kigoma na kujionea namna Maafisa Afya wamejipanga kudhibiti magonjwa ya mlipuko mipakani ambapo amesema Serikali itawachukulia hatua kali wale wote watakaobainika kwenda kinyume na agizo hilo.


“Tusiuze kadi za homa ya manjano kimagendo bila kuchanja, utaratibu upo kuna nchi zimeorodheshwa na mtu akisafiri akitoka katika nchi hizo lazima awe amechanjwa na kuchanjwa maana yake aoneshe uthibitisho wa kadi, sasa kuna wengine wanaingia hawana hizo kadi wanauziwa bila kuchanjwa sio kigoma peke yake naongelea bandari zote tuwe waaminifu katika kutenda kazi zetu, tufuuate taratibu na miongozo kwamba tusitoe kadi za homa ya manjano bila kuchanja” Amesema Prof. Nagu


Pia Prof. Nagu amewataka wataalam wa afya wa mipaka na bandarini kutambua ukubwa wa jukumu ambalo wamepewa na Serikali katika kuhakikisha nchi yetu inabaki salama.


“Tunajukumu kubwa sana lakuhakikisha watu wenye magonjwa ya kuambukiza hawaingii nchini kwetu, na pia tulinde mipaka yetu dhidi ya dawa ambazo sio Sahihi au Feki lakini pia na vifaa tiba, Tunawategemea ninyi sana kuhakikisha mnailinda mipaka yetu”


Aidha Prof. Nagu ameishukuru Mamlaka ya Bandari Tanzania TPA kwa kuendela kutoa ushirkiano kwa Wizara ya Afya hasa katika maeneo hayo jambo linalosaidia kuimarisha usalama wa nchi yetu


“Tushikiane kudhibiti magonjwa na vifaa tiba, Vilivyo vibovu visiingie nchini kwetu lakini pia na sisi kuzuia vitu na madawa yetu kutoroshwa, kwahiyo naomba sana tushirikiane tuendelee kudhibiti tusipate magonjwa ya Mlipuko, dawa zisizo salama, vitendanishi na Dawa ambazo hazina ubora”Amesema Prof. Nagu

Post a Comment

0 Comments