NAIBU KATIBU MKUU MNDEME ACHAGIZA AJENDA YA NISHATI SAFI YA KUPIKIA






Naibu Katibu Mkuu (Mazingira) Ofisi ya Makamu wa Rais Bi. Christina Mndeme amesema ajenda ya kutumia nishati safi ya kupikia ni uchumi kwani inaokoa muda wa kutafuta kuni na kujikita kwenye shughuli za kujiingiza kipato.


Akizungumza kwenye kipindi cha Uhifadhi wa Mazingira (UHIMA) kilichotayarishwa na kituo cha televisheni cha Channel Ten hivi karibuni, amesema nishati safi ya kupikia inaokoa mazingira kwa wananchi kuacha kukata miti kwa ajili ya kuni na mkaa.


Ameeleza kuwa ajenda hiyo ambayo kinara wake ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan inapaswa kuungwa mkono kwa nuvu zote kwani ni muhimu kwa afya ya binadamu na hifahi ya mazingira.


Aidha, Naibu Katibu Mkuu Bi. Mndeme amezungumzia R nne akizihusisha na hifadhi ya mazingira kupitia nishati safi ya kupikia akitaja Upatanisho (Reconciliation) kati ya mwanadamu mmoja mmoja, jamii, Tanzania, Afrika na Dunia kwa ujumla na mazingira.


Amesema mazingira yasipotunzwa kupitia matumizi ya nishati chafu kutasababisha uzalishaji wa hewa chafu ambayo ikisambaa angani inaharibu mazingira, hivyo nishati safi inahimiza matumizi ya nishati safi.


Bi. Mndeme ametaja Ustahimilivu (Resillience) ambapo amesema kwa kutumia nishati safi ya kupikia tutarejesha uoto wa asili uliopotoea kutokana na uchomaji na ukataji wa miti kwa ajili ya kuni na mkaa.


Halikadhalika, amesema kuwa Mabadiliko (Reform) ni R nyingine ambayo ni kuleta mabadiliko katika suala zima la mazingira kwa kubadilisha fikra kuachana na kuni na mkaa na kuanza kutumia nishati safi.


“Ni kweli tumekuwa tukitumia kuni na mkaa katika mapishi sasa inabidi tubadilke tuachane na nishati chafu tuanza kutumia nishati safi ili kuleta mabadiliko kiuchumi na kiafya,” amesisitiza.


Bi. Mndeme amesema Rais Samia anaijenga Tanzania upya (Rebuild) kupitia ajenda ya nishati safi ya kupikia kwa kujenga mitazamo ya jamii kwa lengo la kujenga uchumi.


Amesema taifa kwa ujumla litaondokana na uharibifu wa mazingira na kutokana na hatua hiyo, jamii itaachana na ukataji ovyo wa miti na kuchoma misitu pamoja na wanawake kutotumia muda mwingi kutafuta kuni, kufanya shughuli za kiuchumi.


Kwa upande mwingine ametoa wito kwa wananchi kuacha kuchoma misitu kwa kigezo cha kusafisha mashamba kwani kitendo hicho kinasababisha uzalisha wa gesijoto angani.

Post a Comment

0 Comments