Eneo la boma hilo ambalo halijakamilika ndilo linalotakiwa kubomolewa kupisha eneo la barabara
NA NEEMA NKUMBI -NKUMBI MEDIA
wananzengo wa mtaa wa Korogwe Kata ya Nyasubi wakiwa katika mkutano wa kutatua mgogoro wa mipaka ya barabara
Mwanamke anayelalamikiwa kuingilia mipaka ya barabara
Kaimu Mkuu Idara ya Ardhi wa Wilaya ya Kahama Lameck Evarist akiwaelekeza wananchi mipaka ya barabara baada ya upimaji
Mgogoro wa mipaka ya ardhi ya hifadhi ya barabara uliodumu kwa miaka ishirini na sita sasa umemalizika baada ya idara ya ardhi kufika katika eneo hilo na kufanya vipimo na kuonesha mipaka halisi.
Hayo yamefanyika Juni 19, 2024 ambapo wananchi pamoja na viongozi waliazimia kufanya mkutano na kuwaita idara ya ardhi kwa lengo la kumaliza changamoto hiyo.
Susana Richard ambaye ni mwananchi wa eneo hilo amesema wamehangaika na barabara kwa miaka mingi kabla ya mwananchi huyo kujenga ukuta na alipewa barua iliyomuamuru kubomoa lakini hakufanya hivyo.
"yaani mgogoro huu umekuwa wa miaka mingi kama ni mtoto atakuwa chuoni sasa tunahangaika hatuna pa kupita hii barabara tumehangaika nayo kabla hata hajajenga palikuwa na uzio wa miti aliletewa barua ya kutoa uzio lakini hakutoa akajenga ukuta lakini najiuliza maafisa ardhi ndio wanaoleta barua kwa ajili ya kubomoa lakini hatekelezi kuna nini", alisema Susana
Amani Khalfan amesema mtu mmoja hawezi kuzuia barabara isiwepo ambapo aliiomba ofisi ya ardhi kufanya vipimo ili kujua kama barabara ipo au haipo.
"naiomba serikali waangalie ramani na ifanye vipimo ili watupe mrejesho kwamba hivi viwanja virudi katika mipaka yake na barabara iweze kupatikana kwa sababu tunaweza tukawatunazozana na jirani kumbe barabara haipo", alisema Amani
Kwa upande wake Martha Kimaro ambaye analalamikiwa kuingilia mipaka ameeleza kuwa mgogoro huo umeanza toka mwaka 1998 alijenga uzio baada ya kupimiwa na maafisa ardhi baada ya kujenga, mwaka 2016 walikuja na kubomoa uzio huo.
Amani Boimanda ni mwenyekiti wa Nzengo ya Korogwe Kata ya Nyasubi Manispaa ya Kahama amesema amaufahamu mgogoro huo kwa miaka mingi walianza kufanya mazungumzo kama ndugu lakini mazungumzo hayo hayakusaidia ndipo walipoamua kwenda ngazi za juu.
" tulifanya mazungumzo kama majirani lakini hatukupata mwafaka mzuri tulienda ardhi na Afisa ardhi alipokuja alituelekeza barabara inapita wapi na nani aliyeziba barabara", alisema Boimanda
Baada ya Kaimu Mkuu Idara ya Ardhi wa Wilaya ya Kahama, Lameck Evarist kufika katika eneo hilo kwa ajili ya kutoa tafsiri ya barabara inapotakiwa kupita amesema alama walizoziweka leo ndipo barabara inapotakiwa kupita kwa mujibu wa upimaji hivyo sehemu ya nyumba ya Martha inatakiwa ikatwe.
Hata hivyo Diwani wa Kata ya Nyasubi Wilaya ya Kahama, Abel Shija amesema mgogoro ulikuwa unakwamisha maendeleo ya eneo hilo kwa kuwa mgogoro umeisha barabara hiyo inatarajiwa kuingizwa katika bajeti ya mwaka wa fedha 2024/2025.000
0 Comments