Na. Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura hauhusiani na maandalizi ya uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika mwaka huu wa 2024.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Bw. Kailima, R. K wakati akifungua mkutano wa Tume na Maafisa Habari wa Mikoa na Halmashauri tarehe 15 Juni, 2024 jijini Dar es Salaam.
Mkutano huo unahitimisha mfululizo wa mikutano ambayo Tume imefanya na wadau wake kauanzia tarehe 07 Juni, 2024. Baadae Tume itafanya mikutano na wadau kwenye mikoa yote kwa kuzingatia ratiba ya uboreshaji wa Daftari.
Mikutano hiyo ina lengo la kuwapa wadau taarifa za uwepo wa zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura na kuwapitisha katika vifaa na mifumo ya uandikishaji pamoja na kuona namna zoezi litakavyofanyika vituoni.
Maafisa habari wa mikoa na halmashauri mnalojukumu la kuelimisha wananchi na kuzuia kusambaa kwa taarifa za upotoshaji kama ile inayodai kwamba uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura unahusika na maandalizi ya uchaguzi wa serikali za mitaa, amesema Bw. Kailima.
Mkurugenzi huyo wa uchaguzi amenukuu kifungu cha 10(1)(c) cha Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Na. 2 ya Mwaka 2024 ambacho kinaelekeza kwamba Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi itasimamia uchaguzi wa serikali za mitaa kwa kutumia sheria itakayotungwa.
Kifungu cha 10(1)(c) cha Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Na. 2 ya Mwaka 2024 kinaweka sharti kwa Tume kusimamia na kuratibu uendeshaji wa uchaguzi wa serikali za vijiji, mitaa na vitongoji Tanzania Bara kwa kuzingatia utaratibu utakaoainishwa katika Sheria itakayotungwa na Bunge. Sheria hiyo bado haijatungwa, amesema Bw. Kailima.
Mkrugenzi wa Uchaguzi amewaasa watu wanofanya upotoshaji huo waache kwa kuwa matokeo yake ni mabaya na yanaweza kuathiri mwenendo wa kupiga kura kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa.
Amesisitiza kuwa sheria mbili zilizofutwa ambazo ni Sheria ya Taifa ya Uchaguzi Sura ya 343 na Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa Sura ya 292 hazihusiani na uchaguzi wa serikali za mitaa, hivyo wananchi wawe makini na wapotoshaji.
Sheria ya Taifa ya Uchaguzi Sura ya 343 na Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa Sura ya 292 zilizofutwa zilikuwa zinahusika na uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani. Sio kweli kwamba kufutwa kwa sheria hizo kunaathiri uchaguzi wa Serikali za Mitaa, zipo sheria zinazosimamia uchaguzi wa Serikali za Mitaa, amesema.
Bw. Kailima amezitaja sheria zinazohusika na mamlaka ya usimamizi wa uchaguzi wa serikali za mitaa kuwa ni pamoja na Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Miji) Sura ya 288 na Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Wilaya) Sura ya 287.
0 Comments