MTANDAO wa Jinsia Tanzania (TGNP) umeiomba serikali na tume ya mipango kuzingatia suala la jinsia na kuliweka kama lengo la kujitegemea katika dira ya Taifa ambapo awali yaliachwa nakupelekea jinsi moja kubaki nyuma katika masuala ya mgawanyo wa Mali na rasilimali hata katika suala la Uongozi.
Ombi hilo limetolewa leo Mei 29,2024 Jijini Dar es Salaam, katika zoezi la ukusanyaji wa maoni kwa njia ya dodoso na mijadala,katika makundi mbalimbali ya wanawake vijana wanaopatikana vyuoni na katika ngazi ya jamii.
Akizungumza na waandishi wa habari Afisa Programu na Mipango TGNP Bi.Logathe Lyakaki amesema wamejadili dira ya Taifa ya 2025 ambapo wamebaini mambo mbalimbali kuhusiana na masuala yao yaliyofanikiwa na kuzifahamu changamoto kuhusiana na yale ambayo hayakufanikiwa.
"Kuelekea dira ya 2050 wamesema ni mambo gani ambayo wanatamani yazingatiwe kwa vijana ambapo tutakapokuwa na hiyo dira iwe na sura jumuishi ya makundi yote haswa kundi lao ambalo ni kubwa lenye umuhimu sana katika kuchagiza maendeleo ya nchi" amesema Logathe
Pamoja na hayo, Logathe ameeleza kuwa zoezi hilo limefanyika kikamilifu na wanatarajia kukabidhi maoni yao kwa Mratibu kwa ajili ya kuyawasilisha katika tume ya mipango ambapo wanaamini vipaumbele walivyoviweka vijana vitazingatiwa na kuingizwa katika dira hiyo kwaajili ya kuunda dira jumuishi inayogusa makundi yote.
Kwa Upande wake, Mkurugenzi wa Taasisi ya Bridge for Change Bw. Ocheck Msuva amesema Mkutano huo umelenga kupata maoni ya wanawake vijana kuhusiana na matamanio yao katika dira ya Taifa ijayo na kutambua mtizamo wao katika dira iliyopita ili kuleta maoni yenye tija na ufanisi kwa dira ijayo
Naye,Mwanafunzi wa chuo Kikuu Cha Ardhi Bi.Sarah Julius Mpanda ameipongeza serikali kuweka fursa kwa kila kundi wakiwemo vijana kutoa maoni yao katika dira ya Taifa katika nyanja ya kiuchumi kijamii na kisiasa.
Vilevile, Mwanafunzi wa Chuo Kikuu St. Joseph,Ziada Aman ameeleza kuwa wametoa maoni katika nyanja ya kiuchumi, kijamii na kisiasa ambapo katika Upande wa uchumi wameshauri kupunguzwa kwa Kodi kutokana na kipato cha watu husika katika maeneo ya mjini na vijijin
Zoezi hilo la ukusanyaji maoni linaratibiwa na shirika lisilo la kiserikali la United Nation Association of Tanzania (UNAT) ambao wamepewa dhamana na tume ya mipango,kuratibu na kukusanya maoni katika makundi mbalimbali.
0 Comments